19 Septemba 2024 - 11:04
Idadi ya Mashahidi katika milipuko ya Jumatano nchini Lebanon imeongezeka hadi kufikia Mashahidi 20

Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa zaidi ya watu 450 walijeruhiwa katika milipuko ya Jumatano katika nchi hii.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul_Bayt (a.s) - ABNA - Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza ongezeko la idadi ya Mashahidi na waliojeruhiwa katika milipuko ya Jumatano nchini humo hadi kufikia Mashahidi 20 na watu zaidi ya 450 kujeruhiwa.

Waziri wa Afya wa Lebanon "Firas Al-Abeid" alisema kuwa majeraha mengi ya waliojeruhiwa katika milipuko ya Jumatano yalikuwa ya juu juu (ya kawaida) na wengi wa waliojeruhiwa waliruhusiwa kutoka Hospitalini.

Aliendelea kusema: Msaada wa haraka wa matibabu umefika nchini Lebanon kutoka katika baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Iraq na Jordan.

Hali katika Hospitali za Lebanon imedhibitiwa na tuko tayari kutekeleza mipango ya dharura ili kukabiliana na matukio yoyote.

Inafaa kutaja kwamba 'Vyanzo vya Habari' viliripoti sauti ya milipuko iliyofuatana katika viunga vya Beirut na maeneo mengine huko Lebanon mnamo Jumatano tarehe 18 Septemba, 2024.

Katika milipuko hii, sambamba na simu zisizotumia waya, simu zingine za mezani, vifaa vya Laptop na baadhi ya vifaa vingine (vya Kielektroniki) vya mawasiliano vililipuka, ambapo milipuko hii ilisababisha hasara na uharibifu mkubwa.

Pia, kutokana na matokeo ya milipuko hii, moto mwingi ulitokea katika nyumba za makazi, maduka na magari katika sehemu tofauti za Lebanon.